UKIFIKA
katika mtaa anaoishi mwanamuziki Diamond maeneo ya Sinza Mori jijini
Dar es Salaam utaanza kuhisi kuwa kuna staa anayeishi maeneo hayo, macho
ya wengi huanza kumtazama mtu anayeelekea katika geti la nyumba
anayoishi msanii huyo. (HM)
Muda wote geti hilo limefungwa. Ili
uweze kuingia ndani itakulazimu ubonyeze kengele itakayoashiria kuwa
kuna mgeni nje anahitaji kuingia ndani. Hata hivyo hauwezi kupenya
kirahisi ndani hadi uulizwe shida yako na kama hauna miadi na mtu yeyote anayeishi ndani ya nyumba hiyo haitakuwa rahisi kuingia.
na kushuhudia ukimya wa hali ya juu
ilhali kuna watu ndani. Baada ya kufunguliwa geti tuliingia ndani na
kupokewa na Diamond aliyekuwa ameketi katika sebule iliyonakshiwa na
mapambo makini ukutani huku ikiwa na samani chache lakini za gharama
kubwa.
Tulitumia saa mbili mfululizo katika
mahojiano na Diamond ambaye alifunguka kwa kila swali aliloulizwa na
kujibu kwa ufasaha na ufafanuzi mpana.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje katika muziki?
Diamond: Nina mipango makini
katika kazi zangu. Mambo yote lazima yapitie kwa meneja wangu ndipo
yanifikie mimi, mara nyingi mtu hawezi kuzungumza na mimi moja kwa moja
lazima apite huko na hiyo ndiyo staili ya Diamond. Nimejipanga
kuhakikisha nafanya kazi gani, kwa wakati gani na sikurupuki tu, japo
katika utengenezaji wa nyimbo zangu naweza nikapata wazo basi hapo hapo
nikatengeneza mistari.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje kuanzia asubuhi hadi jioni?
Diamond: Saa tano asubuhi,
nikishaamka kitu cha kwanza ni kwenda 'gym', mara nyingi ni hapa
nyumbani kama unavyoona hapo nje kuna sehemu ya mazoezi na sehemu
nyingine zilizopo ndani, mara nyingi
hutumia muda wa saa moja. Ifikapo saa sita na nusu huwa naanza kufanya
kazi zangu lakini itategemea na ratiba zangu za siku ambazo ndio
mwongozo wangu wa kuimaliza siku. Baada ya hapo napumzika kwa muda
fulani na baadaye jioni huendelea na kazi na mara nyingi kazi zangu huwa
nazimaliza usiku wa manane.
Mwanaspoti: Unalala saa ngapi? Na unalala kwa muda gani?
Diamond: Muda wangu wa kulala
mara nyingi ni saa kumi na moja alfajiri na kama sikuwa na kazi nyingi
studio basi nitalala saa nane usiku. Muda wangu wa kulala ni saa sita
mpaka nane kwa siku. Ila hata kama nikilala mapema kuamka ni saa tano
asubuhi ila itategemea na nini ninakifanya siku inayofuata na kama nina
kazi maalumu na ya mapema itanilazimu niamke mapema ili kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Shughuli gani zinazokuchelewesha mara kwa mara kulala?
Diamond: Ni kurekodi na wakati
mwingine shoo. Kwa wiki ninafanya shoo nyingi, kama ni tatu basi siku
zote tatu nitalala alfajiri. Siku nyingine zinazosalia ninalala usiku wa
manane kwa kuwa huwa nakuwa studio na sehemu nyingine ambazo hunilazimu
kufanya kazi kwa kipindi kirefu usiku.
Mwanaspoti: Kati ya usiku na mchana ni muda upi unaopenda kurekodi?
Diamond: Kazi zangu narekodi
usiku na ndiyo muda ninaopendelea zaidi. Mara nyingi napenda kurekodi
saa 7 usiku ili niwe na muda na saa nyingine ni kuepuka lawama kurekodi
mchana, kwasababu vijana wengi chipukizi wataona napendelewa. Unajua
ninapoingia studio napenda kufanya kazi kwa muda mrefu, hata hivyo iliyo
bora sifanyi bora liende na siwezi kufanya kazi na prodyuza
anayenipeleka tu, ni lazima na mimi nipime kama kazi niliyoifanya
inakwenda vile ninavyotaka au kama yeye anavyotaka ilimradi tufanye kazi
nzuri na iliyo
bora.
Mwanaspoti: Unatumia muda gani kurekodi singo moja na kwa upande wa video ni siku ngapi?
Diamond: Inategemea, inaweza kuwa
siku mbili au miezi sita lakini nyimbo nyingi zinatumia muda mwingi
kwasababu wakati mwingine naanza halafu napata shoo hivyo inanibidi
nipange muda mwingine wa kurekodi. Kuna nyimbo zangu ambazo nilizifanya
kwa muda mrefu sana hizo huwa sizisahau ikiwemo Ukimwona, Mbagala,
Nataka Kulewa na nyinginezo. Nakumbuka katika kazi nilizofanya kwa muda
mfupi ni My Number One nilioufanya kwa prodyuza Sheddy Clever kwa
kipindi kifupi sana pamoja na Mapenzi Basi sambamba na Binadamu hizi ni
baadhi ya kazi ambazo hazikunipasua sana kichwa kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Una prodyuza wako maalumu au studio yako mwenyewe?
Diamond: Sina prodyuza maalumu
kila kazi nitakayotaka kuifanya ninatafuta prodyuza yule ninayemtaka
hata kama sijawahi kufanya naye kazi. Ninafanya hivi nikiwa na malengo
maalumu kwa kujiweka vizuri mimi kama msanii na hata kuwapa nafasi
maprodyuza mbalimbali kutia mkono kwenye kazi ya mikono yangu. Ninaogopa
kuwa na prodyuza maalumu kwa kuwa najua atanisumbua ikiwa atajua kwamba
namtegemea yeye pekee katika kazi zangu. Studio sina kwa sasa ila nina
mikakati ya kuwa na studio kwani nimeshanunua baadhi ya vifaa.
Mwanaspoti: Unadhani ndiyo sababu iliyokufanya ukagombana na Bob Junior au Manecky?
Diamond: Hapana haya mambo
yalishapita lakini nilijifunza mengi ndiyo maana niliamua kuja na staili
hii. Naogopa kubaki kuwa msanii ninayetegemea prodyuza fulani, bila
yeye siwezi kufanya muziki, lakini mimi ni Diamond ninaweza kufanya
muziki na prodyuza yeyote naye akaonyesha ufundi wake kupitia kazi
yangu.
Mwanaspoti: Shoo gani kubwa kuliko zote uliyowahi kufanya ambayo haijawahi kujirudia?
Diamond: Diamond Forever. Hii
ilikuwa kubwa sana ambayo sitakaa nikaisahau, ilihudhuriwa na watu
wakubwa na maarufu hapa nchini hata hivyo ilikuwa ya kipekee ambayo
haijafanana na yoyote ile. Ya pili ni ile ya Dar Live ambayo nilifanya
baada ya kushuka katika helikopta ile pia ilikuwa kubwa. Lakini kwa nje
ya nchi ni Mombasa na Comoro huko nilifanya shoo kubwa sana ambazo
siwezi kuzisahau.
Mwanaspoti: Ni shoo ipi iliyowahi kukuingizia pesa kubwa kuliko zote?
Diamond: Shoo ile ya Mlimani City
ya Diamond Forever, ile iliniingizia pesa kubwa sana na tangu pale
ndipo nilipoanza kufurahia matunda ya kazi yangu. Nilifanya shoo pia
Burundi, Mombasa na Congo shoo hizi ziliniingizia kiasi kikubwa sana cha
pesa siwezi kutaja ni shilingi ngapi lakini ni pesa nyingi ambazo
sitakaa nizisahau.
Mwanaspoti: Shoo ipi ilikuwa ya bei chee ambayo huwezi kuisahau
Diamond: Kwa kweli siwezi kusahau
nilipofanya shoo yangu ya kwanza kubwa mwaka 2009 kwenye Fiesta
iliyofanyika Dar es Salaam, ilikuwa ndiyo shoo yangu ya kwanza na kubwa
wakati huo nilikuwa natamba na wimbo Kamwambie, ilinichukua muda mrefu
sana kujiandaa mimi pamoja na madansa wangu wanne tulilipwa Sh 50,000
lakini sikukata tamaa kwani ilikuwa ndiyo mwanzo wangu wa kujuana na
watu wengi na wadau wakubwa wa muziki hapa nchini ambao nilikutana nao
kwenye ile shoo.
Mwanaspoti: Kwa hivi sasa ni shoo gani ambayo unaweza kusema kwamba utafanya kwa bei ya chini na ni shilingi ngapi?
Diamond: Shoo ninayoweza kufanya
kwa bei ya chini kabisa ni Sh 10 milioni za Kitanzania na hii labda
nione anayeniomba nifanye shoo hiyo hayuko vizuri na pengine ni rafiki
yangu na hawezi kuninyonya, si hivyo tu itategemea pia ni kampuni gani
na ni watu wa aina gani ambao watanitaka nifanye nao kazi.
Mwanaspoti: Kwa kawaida Diamond ni msanii wa gharama gani kwa shoo moja ndani na nje ya nchi?
Diamond: Kwa kawaida shoo moja
ninafanya kuanzia Sh15 milioni mpaka Sh20 milioni kulingana na muda
nitakaofanya shoo. Pia zile za nje ninafanya kwa gharama ya Dola 20,000
mpaka 30,000 yaani ni Sh32 milioni mpaka 48 milioni hivi kwa fedha za
Tanzania na nikiwa huko nahakikisha ninafanya kazi vile inavyotakiwa.
Lakini hali ni tofauti inavyokuja shoo ile ya uwanjani yaani hapa
nazungumzia shoo kubwa zinazofanyika nje ya ukumbi, hizi natoza Dola
20,000 ambayo ni sawa na Sh32 milioni 32 kwa fedha ya Kitanzania.
Mwanaspoti: Kuhusu madansa wako unawachukuliaje?
Diamond: Ni kama kaka zangu na
ninawapenda sana kwani tumetoka nao mbali na wanajua kuwa tunafanya kazi
pamoja kutengeneza maisha hivyo ni kama ndugu zangu na tunasaidiana
kwenye kila jambo ukizingatia kuwa kile tunachokipata tunagawana. Kwa
kweli najitahidi sana kuwaambia hasa kuhusiana na masuala ya kimaisha,
nahusika katika maisha yao ya kila siku na nijuavyo mimi nikikosea tu
mmoja akapotea kundi langu litakuwa limeharibikiwa maana kila mtu
namtegemea kwa upande wake. Kwa sasa wamejenga nyumba zao na wanaendelea
vizuri kimaisha hilo ndilo sharti langu lazima wafanye mambo ya
maendeleo kwa kile tunachokipata.
Mwanaspoti: Umesafiri nao nchi ngapi, na kwanini unapenda kuambatana nao?
Diamond: Nimesafiri nao sehemu
mbalimbali kama Burundi, Comorro na sehemu nyinginezo ambako nimekwenda
kufanya shoo, sina tabia ya kusafiri peke yangu hata nikienda Ulaya na
hata Marekani lazima niwe nao. Ninapenda kuwa nao kwani ni sehemu ya
muziki wangu na imefika wakati nimekuwa nataka mapromota kuhakikisha
wanatulipia mimi na madansa wangu kwa ajili ya shoo hasa tutakapojua
kuwa shoo fulani itaingiza watu wengi au udhamini mkubwa.
Mwanaspoti: Kuna safari ambayo umewahi kusafiri peke yako?
Diamond: Ziko nyingi, nilienda
mwenyewe kutokana na ukubwa wa shoo, lakini ni miaka kadhaa nyuma,
baadaye nilijiwekea mikakati kwamba siwezi kusafiri mwenyewe wakati shoo
nahitaji kufanya na madansa wangu, awali mapromota walikuwa wagumu
kunielewa na wapo waliokataa. Niliachana nao na kuwataka wakishajipanga
na kuhakikisha kwamba wanaweza kunichukua mimi na madansa wangu
watafanya hivyo.
Mwanaspoti: Umewahi kuwatema madansa?
Diamond: Sijawahi kubadilisha
madansa kwa sababu wanajua kazi yao. Ingawa nilikuwa na madansa sita
nilipokuwa naanza muziki lakini niliachana na wawili kutokana na
utendaji wao wa kazi. Wawili hawa hawakuwa wabunifu kila siku walikuwa
na staili ileile, niliamua kuchagua vichwa ambavyo vikikaa na mimi
mwishowe tunatoka na kitu makini na chenye kueleweka. Kulikuwa na tatizo
pia la kukosea stepu wakati wa shoo hili lilikuwa likinishushia sana
hadhi yangu jukwaani, hapo ndipo nilipoamua kuwaondoa.
Mwanaspoti: Kwa upande wa malipo unawalipaje?
Diamond: Ninawalipa vizuri lakini
siwezi kutaja kiwango ila ingekuwa kwangu ningetaja, hiyo ni haki yao
wao wenyewe kutamka ila mimi siwezi kutaja. Malipo ninayowalipa yapo
machoni mwa watu wanaowazunguka, dansa kujenga nyumba kumiliki baadhi ya
biashara si jambo dogo, hivyo ninawalipa vizuri. Na hata gharama za
kusafiri ndani na nje ya nchi vyote ni juu yangu, malipo tunayoyapata
tunagawana.
Mwanaspoti: Unakumbana na changamoto zipi katika kazi yako?
Diamond: Nakumbana na mengi,
kwanza unapokuwa msanii unayeongoza lazima upate vikwazo vingi.
Nakumbana na watu wengi wanaonichukia na kunitusi bila sababu za msingi,
hata hivyo nasingiziwa vitu vingi ambavyo havipo nadhani hii ni
changamoto iliyotokana na kufanya vizuri katika muziki.
Wapo ambao wanamwona Diamond anafanya
vizuri kwenye muziki badala ya kukaa na kuangalia nimepita wapi na wapi
anaanza kutoa lawama kwamba ameibiwa na mengine ambayo kimsingi hayana
maana.
Mwanaspoti: Siku za hivi karibuni
kuna maprodyuza na wasanii wasiofahamika ambao walijaribu kutengeneza
kazi yako ya My Number One na kukutusi kupitia wimbo huo na wapo
waliotunga mashairi mengine yaliyozungumzia maisha yako kabla hujawa
staa, ulijisikiaje? Na unachukua hatua gani?
Diamond: Awali niliumia sana
nilipoibiwa mashairi ya wimbo wangu wa Mbagala, iliniuma sana kwa muda
wa wiki nzima uchungu nilioupata siwezi kuuelezea. Lakini baadaye
nilikomaa, huwezi amini niliposikia zile nyimbo nilicheka sana kisha
nikawadharau sana watu waliofanya hivyo maana nipo kwenye hii tasnia
siwezi kuchukia watu wasiojua walitendalo kwani na wao wapo katika
kujitafutia riziki. Lakini hata hivyo sheria ya muziki bado haijawa
makini hapa nchini
nitachukua hatua gani mwisho wa siku
nitaacha kufanya mambo yangu ya msingi na kushughulikia wezi wa kazi
zangu ambao hata hivyo hawatabanwa kwa lile walilolifanya.
Mwanaspoti: Msanii yupi hapa Tanzania anakutisha kama hayupo vipi huko nje ya nchi?
Diamond: Kwa hapa Tanzania
sijaona mwanamuziki anayenitisha, ila siwezi kujua mashabiki wao ndio
majaji, nafikiri kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake. Kati ya
wanamuziki ninaowahusudu mimi kwa nje ya nchi hasa Afrika ni P Square
pekee, hawa wapo katika nafasi kubwa sana kwenye ubongo wangu na
nafikiria ni lini ninaweza kuwafikia, hiyo ndiyo ndoto yangu daima.
Mwanaspoti: Unapokuwa juu ya jukwaa unakumbana na vishawishi vipi ukiwa kama msanii mkubwa?
Diamond: Ninapata vishawishi
vingi sana ninapokuwa jukwaani. Kwa kweli ninashawishiwa na wakinadada,
mfano kuna mwanamke mmoja ambaye alikuwa mmoja wa mapromota wa shoo
nchini Uingereza alitaka kunibusu mdomoni kwa lazima, kitendo kile
kilinifedhehesha sana na nilishindwa nifanyeje kwani nipo ugenini na
jukwaani ilikuwa ngumu sana kwangu. Wakati mwingine wanawake wanapanda
jukwaani ili wacheze na wewe mwisho wa siku wanaingiza mikono kwenye
suruali yaani sipendezwi kabisa na michezo ya namna hii.
Mwanaspoti: Umewahi kuibiwa ukiwa jukwaani?
Diamond: Nimeshaibiwa sana hasa
katika hizi shoo ndogo ndogo mara nyingi watu wanapanda jukwaani na
kuondoka na kitu chako. Nakumbuka nimeshawahi kuibiwa saa, pete ya
dhahabu na kuna mmoja alitoa kali ya mwaka yaani yeye alinivua nguo kwa
lazima.
Mwanaspoti: Inakuwaje nje ya muziki, unakumbana na changamoto zipi?
Diamond: Kitu ambacho ni
changamoto kubwa sana kwangu ni simu yangu ya mkononi. Kila baada ya
miezi sita au mitatu nalazimika kubadili namba yangu ya simu,
nasumbuliwa sana na watu ambao hata hivyo hawana la msingi la kuniambia.
Ni kweli kwamba mawasiliano ni kitu cha msingi na
ninawapenda mashabiki wangu lakini namba
yangu inasambaa kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba nashindwa kupokea simu
za maana kwa kudhani kwamba na hao nao ni wasumbufu.
Mwanaspoti: Ina maana milio yote ya simu hapo ni watu wanakupigia?
Diamond: Yap, unavyoona inalia
kila dakika watu wanapiga hapa. Muda mwingi hii simu ninaweka 'silent'
yaani haitoi mlio wowote kwani inaita kila dakika.
Mwanaspoti: Tuzungumzie uhusiano wako. Mpenzi wako wa kwanza unamkumbuka? na je uliwahi kumpa shilingi ngapi?
Diamond: Mpenzi wangu wa kwanza
kabisa enzi hizo ninajifunza mambo haya sikumbuki vyema jina ila alikuwa
anaishi Tandale na mimi pia nilikuwa naishi huko na mama yangu.
Sikumbuki kama nimewahi kumhonga maana enzi hizo mimi nilikuwa napewa tu
na mama yangu pesa, sikuwa na hela yoyote ya kumpa na ilikuwa ni kwa
kipindi kifupi kama miezi minne hivi, hata hivyo tulikuwa tunaibana tu
kwa siri nilikuwa mdogo.
Mwanaspoti: Kwanini mliachana?
Diamond: Kwanza nilikuwa sijajua
mapenzi ni nini. Hata hivyo haikuwa rasmi na wala nilikuwa sijawa na
akili ya kupenda sana na nilikuwa na fikra kwamba ni mchezo tu hivyo
tuliachana mapema kwani hata yeye akili yake ilikuwa haijakomaa.
Mwanaspoti: Mpenzi wako uliyekuwa naye kabla ya kuwa staa nasikia uliachana naye baada ya kutoka kimuziki kwa nini?
Diamond: Nilimpenda sana lakini
aliniacha kabla ya kutoka. Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa anaitwa Sarah
Sadick, sijawahi kumuhonga na ndiye mwanamke niliyewahi kumpenda sana.
Wakati huo Naseeb Abdul kabla sijawa Diamond nilikuwa nahaha kuhangaika
ni vipi nitatoka kimuziki. Msichana huyu ndiye aliyenipa hasira za
kufanya muziki kwa bidii zote baada ya kunitema na kuanza kuhangaika na
wengine na aliniita majina mengi yasiyo mazuri, kisa sina fedha. Si
kwamba nilimuacha bali yeye ndiye aliyeniacha kama zali baada ya wiki
kadhaa nikatoka na wimbo Kamwambie, taratibu nikaanza kuwa staa naye
akaanza kurudi ila nilishamuondoa moyoni mwangu.
Mwanaspoti: Kwa nini mliachana? Unadhani hakukufaa tena kwa kuwa ulishakuwa staa?
Diamond: Alinisumbua sana
kutokana na ugumu wa maisha niliokua nao kwa kipindi cha nyuma hadi
kufikia 2009. Nilimpenda sana huwezi amini nilikuwa silali usingizi kwa
ajili yake. Nahisi ilitokana na mimi kukosa kazi ndiyo maana ilifikia
hatua alinipotezea. Lakini baada ya kupata na kujulikana alinifuata
lakini sikutaka tena hata baada ya kuniomba msamaha.
Mwanaspoti: Umewahi kuwa na wanawake wangapi tangu uwe staa?
Diamond: Sikumbuki kwa kweli wapo
wengi mno, si unajua tena wapo walionitaka na kunilazimisha nifanye
hivyo, lakini idadi kamili siwezi kukumbuka na kila siku nasumbuliwa na
hawa wanawake.
Mwanaspoti: Ni wapenzi wangapi ambao umekuwa nao kipindi kirefu na kuwapenda kama wapenzi wako?
Diamond: Nimewahi kuwa na wapenzi
wanne katika kipindi chote cha ustaa wangu na sikupenda kubadili ovyo
ila wengi wao hawakuweza kutimiza haja ya moyo wangu.
Mwanaspoti: Unaweza kuwataja majina?
Diamond: Ndiyo ila wawili
wanafahamika zaidi. Wa kwanza kabisa alikuwa anaitwa Sarah na wa pili
alikuwa anaitwa Hawa yule msichana niliyeimba naye katika wimbo
'Nitarejea', huyu alizidiwa ujanja na Wema Sepetu ambaye naye alikuja
kuondoka kwangu na baadaye nikawa na Penieli Mungilwa.
Mwanaspoti: Mwanamke yupi unahisi ulimpenda kuliko wote?
Diamond: Mwanamke wangu wa kwanza
Sarah Sadick huyu aliniingia sana moyoni sijajua ni kwanini. Lakini
nahisi huenda kwa kuwa awali alinipenda kweli kwa kuwa wakati huo sikuwa
na kitu. Hata hivyo nahisi ilitokana na mimi kutokuwa bize na wakati
huo sikufikiria lolote zaidi ya yeye ilitokana na kutokuwa na kazi ya
kufanya. Siku hizi sina mapenzi ya kivilee, nawaza zaidi pesa na
ninaihangaikia na zaidi ni muziki wangu, hili ndilo la kwanza kabisa
linalonifanya niwe bize mapenzi baadaye.
Mwanaspoti: Umeshawahi kutongozwa na wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena
kuna mmoja kati ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye
mwenyewe ndipo nikawa naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi
kirefu tu. Wanaweza kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini
ukweli ninao mimi mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa
sana kwenye mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp, Instagram na
kwingineko na wapo wasichana ambao wanatafuta namba zangu za simu na
kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Unapata usumbufu wowote toka kwa wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena
kuna mmoja kati ya wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye
mwenyewe ndipo nikawa naye na nilikaa naye katika uhusiano kwa kipindi
kirefu tu. Wanaweza kumfikiria mwanamke fulani lakini huwezi amini
ukweli ninao mimi mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa
sana kwenye mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp, Instagram na
kwingineko na wapo wasichana ambao wanatafuta namba zangu za simu na
kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Ni mwanamke wa aina gani unataka awe mkeo?
Diamond: Kwanza ninahitaji aijue
kazi yangu na ajue kwamba mimi ni mtu maarufu hivyo akubaliane na
changamoto mbalimbali atakazokumbana nazo kwa kipindi atakachokuwa ndani
ya ndoa, siyo siku mbili anafungasha virago. Pia ajue kwamba
nitamsikiliza mama yangu kwanza kabla ya yeye hilo naliweka wazi, yeye
ana nafasi yake katika maisha yangu lakini mama yangu nimempa
kipaumbele, tatu awe tayari kuishi na mama yangu. Nne awe na akili na
mwenye utambuzi na atakayeniongoza katika kazi zangu, sihitaji.
Itaendelea…
Chanzo: mwanaspoti
No comments:
Post a Comment