AUNT Ezekiel ni muigizaji wa filamu mwenye jina kubwa, linaloenda sambamba na muonekano wake wenye mvuto, hasa anapovaa mavazi yake yanayoonyesha baadhi ya sehemu muhimu za mwili wake.
Kwa wasiomfahamu vizuri, Aunt ni mtoto wa mwanasoka mahiri wa zamani wa Simba na Taifa Stars, marehemu Ezekiel Greyson, maarufu zaidi kwa mashabiki wa kabumbu kama Jujuman. Alitamba katika miaka ya sabini na mwanzoni mwa themanini.
Ni mmoja wa wasichana waliofanikiwa kupata majina makubwa, ingawa uwezo wake kama muigizaji, bado haujakidhi viwango!
Hivi karibuni Aunt, mke wa mfanyabiashara Sunday Demonte, kijana wa Kitanzania anayefanyia shughuli zake Ughaibuni, alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema kuwa haogopi kukutwa na skendo, kwani hilo ni jambo la kawaida.
“Mimi sijali, ninachoangalia ni kuingiza kipato, mambo mengine shauri yao, kuna watu wananichukia na kunitungia uongo, huwezi kupendwa na kila mtu, msanii ni kioo cha jamii, lazima upate skendo ili uweze kujirekebisha,” Aunt alinukuliwa akiliambia gazeti hilo.
Ninazifahamu kidogo kazi alizoshirikishwa, nyingi kati ya hizo akicheza na marehemu Steven Kanumba. Aina ya uigizaji wake haubadiliki, ni Aunt yule yule anayependa kuvaa nguo zenye kuonyesha nje sehemu kubwa ya matiti yake, maungo yake na hata mavazi yake mara zote ni yenye utata mkubwa.
Muigizaji mzuri ni yule mwenye kubadilika. Leo anaweza kucheza vizuri kama changudoa, kesho yake akafiti kiufasaha kabisa kama mtoto yatima anayeishi katika umaskini mkubwa, kabla ya keshokutwa kumkuta akiigiza vyema akiwa ni msomi mwenye mafanikio makubwa kimaisha!
Sifa hizo Aunt Ezekiel, kama walivyo mastaa wengi wa Tanzania katika filamu, hana. Ni muigizaji wa kuigiza matanuzi, demu bomba mwenye mitoko mingi, mikogo na mambo kama hayo, ndiyo maana hata mavazi yake, uigizaji wake ni wa aina ileile katika filamu zote alizocheza!
Anasema haogopi skendo, anajali kuingiza kipato. Anahitimisha kwa kukiri kwamba skendo ni jambo la kawaida kwa mastaa, kwani kwa kutokea hivyo, ndipo wao hupata nafasi ya kujirekebisha!
Hawa ndiyo aina ya wasanii tulio nao, wenye wafuasi lukuki mtaani, wanaosimama na kusema wazi kuwa hawaogopi skendo. Mtu makini na hasa anayetakiwa kuwa mfano, hawezi kuwa haogopi skendo!
Ndiyo maana kumbe kila siku tunasikia, mara kapiga picha za nusu utupu na kuzitupia katika mitandao ya kijamii ili watu waone ‘figa’. Mara amepigana na mwenzake club (bila chanzo hasa cha ugomvi kuelezwa, ingawa ni rahisi kuamini walikuwa wakigombea bwana).
Ninaheshimu maoni yake ya kutoogopa skendo, lakini napingana naye kwa kauli kuwa ni kawaida kwa mastaa kupata skendo. Siyo kweli. Wapo mastaa wakubwa, tena wale wanaojua kazi, lakini hawajawahi kuwa mabingwa wa skendo.
Riyama Ally ni mmoja ya waigizaji ‘wanaojua’ kwa levo za Bongo, lakini siwezi kumuweka katika orodha ya wauza sura wanaotumia tasnia kwa malengo yao binafsi.
Wasanii wetu wanaponzwa na uwezo wao mdogo wa ubunifu, ndiyo maana bado wanaamini katika skendo ili kuwaweka juu. Mtu anajisikia vizuri akiandikwa gazetini, bila kujali anaharibu vipi ‘image’ yake kwa jamii. Eti wanasingiziwa, hivi kuna mtu gani makini anaweza kukubali kunyamaza gazeti linapoandika uongo dhidi yake?
Kuna namna moja tu unayoweza kuwazungumzia hawa mastaa wetu wa aina hii, kwamba wanatengeneza skendo makusudi ili wavutie macho na masikio ya wahanga wa ngono!